Advertisement

Responsive Advertisement

​NLD Yaipongeza Ofisi ya Msajili kwa ‘Kuilima’ Barua CCM na CHADEMA

NLD Yaipongeza Ofisi ya Msajili kwa ‘Kuilima’ Barua CCM na CHADEMA

 *Katibu Mkuu Doyo Hassan adai hatua hiyo imerejesha imani: "Sheria sasa ni msumeno."


 * Awatahadharisha wanasiasa wanaochochea taharuki na kashfa kwenye jamii.

 

**TANGA** — Chama cha National League for Democracy (NLD) kimepongeza hadharani hatua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa kuvitaka vyama vya CCM na CHADEMA kujieleza kufuatia msururu wa kauli tata zilizotolewa na makada na viongozi wao hivi karibuni.


NLD imetaja hatua hiyo kama kielelezo cha ukomavu mkubwa wa kisiasa na uwepo wa uwanja sawa wa kisheria kwa vyama vyote, bila kujali ukubwa au ushawishi wao.


Akihojiwa na waandishi wa habari jijini Tanga leo Mei 24, Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema hatua hiyo imesaidia kuzima minong'ono ya uwepo wa upendeleo katika usimamizi wa vyama vya siasa nchini.


Doyo amebainisha kuwa kuandikiwa barua kwa vyama hivyo viwili vikubwa—chama tawala na chama kikuu cha upinzani—kunatoa ujumbe mzito kwa wanasiasa wote nchini.


 "Tumeona Msajili amewachukulia hatua CHADEMA kwa kuwaandikia barua ili wajieleze kutokana na makosa yanayowakabili. Lakini kikubwa zaidi na chenye kuleta matumaini, tumeona Msajili akichukua hatua kama hizo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili nao wajieleze kutokana na matamshi ya kada wao," alisema Doyo .


Mbali na pongezi hizo, Katibu Mkuu huyo wa NLD ametoa onyo kali kwa wanasiasa na vyama vya siasa vinavyotumia majukwaa kutoa kauli zinazoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa nchi.


"Niwaombe wanasiasa nchini pamoja na vyama vya siasa, kuheshimu taratibu na Sheria za Vyama vya Siasa. Tukifuata taratibu tutaondoa mikanganyiko na sintofahamu ambazo huleta taharuki katika jamii," alisisitiza kiongozi huyo.

Post a Comment

0 Comments